TUTUMIE MAONI AU HABARI KUPITIA EMAIL: clickhabari@gmail.com AU SIMU: +255 7557 758 909, : CCM MBELE KWA MBELE 2015

Kizungumkuti CCM, JK awataka wagombea wasinune.


Dodoma/Dar. Rais Jakaya Kikwete amesema idadi ya wanachama wa CCM waliojitokeza kuwania urais ni kubwa, hivyo ni lazima wawape viongozi muda wa kuwachuja lakini akawataka wasiwanunie baada ya kufanya uamuzi.
Rais Kikwete alisema hayo jana katika hotuba yake ya kuvunja Bunge ambayo iliibua waziwazi ushabiki kwa wagombea, hasa baada ya kumtaja aliyekuwa waziri mkuu wake wa kwanza, Edward Lowassa kwa ajili ya kumshukuru.
Akitoa salamu zake kwa wagombea hao, Rais Kikwete aliwapongeza na kuwatakia mafanikio mema katika safari yao.
“Wale wanaogombea urais waliomo humu (bungeni) nawatakia kila la kheri na nawashukuru kwa kuonyesha nia ya kunipokea mzigo huu mzito. Nawatakiwa heri katika matamanio yenu,” alisema Rais Kikwete ambaye aliingia Ikulu mwaka 2005.
“Mko wengi, wote ni vigogo na mmetupa kazi kama kamati kuwachuja kwa hiyo msitununie tukifanya maamuzi.”
Lowassa afunika
Wakati akihitimisha hotuba hiyo, Rais aliwashukuru watu mbalimbali waliofanya kazi kwenye Serikali yake, lakini hali ilikuwa tofauti alipomtaja Lowassa ambaye alifanya naye kazi kwa miaka miwili.
Alimshukuru pia, Makamu wake, Dk Mohamed Gharib Bilal, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na baadaye wabunge na viongozi wengine.
Alianza kwa kuwashukuru huku akiwataja majina. Kila alipotaja majina ya viongozi hao, wabunge walipiga makofi kwa kugonga meza zao. Hata alipomtaja Dk Bilal na Pinda, wabunge hao walishangilia kwa kawaida.
Hata hivyo, alipofikia kutaja jina la Lowassa, kelele za wabunge zilikuwa maradufu, wengi wao wakipiga meza kushangilia, hali iliyomfanya Rais Kikwete anyamaze kwa sekunde kama 50 na ndipo Lowassa aliposimama na kuinamisha kichwa kuonyesha kukubali shukrani hizo.
Wabunge waliendelea kumshangilia hadi alipoketi na ndipo Rais Kikwete akaendelea kutoa shukrani kabla ya kuhitimisha hotuba yake ya saa mbili na dakika 20.
Awaweka wagombea gizani
Kuahirishwa kwa vikao vya juu vya uchujaji makada wanaowania kugombea urais kwa tiketi ya CCM, kumesababisha wagombea, wapambe wao na wanachama kubaki gizani kwa kutoelewa  kinachoendelea na hivyo kutoa nafasi ya kuenea uvumi na ubashiri wa aina mbalimbali.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa awali na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye vikao vya juu vya uchujaji wa wagombea vilikuwa vianze juzi, kwa Kamati ya Usalama na Maadili kujadili taarifa za wagombea urais na kutoa ushauri kwa Kamati Kuu. Taarifa zilizopatikana jana jioni zilieleza kuwa kikao hicho kilitarajiwa kuanza usiku wa jana ingawa kulikuwa na utata mkubwa.
Ratiba hiyo ilionyesha kuwa kikao cha Kamati Kuu kilikuwa kifanyike jana, lakini kutokana na sababu zisizojulikana hakikufanyika na badala yake imeelezwa kitafanyika leo, siku ambayo ilikuwa imepangwa rasmi kwa ajili ya mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) unaojumuisha wajumbe zaidi ya 400.
Kwa mujibu wa ratiba hiyo, Mkutano Mkuu wa CCM ambao ndiyo wenye jukumu la kutoa mgombea urais, ulipangwa kufanyika kesho na keshokutwa, lakini taarifa zilizopatikana baadaye zilisema utafanyika kwa siku moja tu ya kesho.
Nape alipotafutwa mara mbili kwa nyakati tofauti jana, majibu yake yalikuwa mafupi; “ratiba niliyotoa ndiyo hiyohiyo, ifuateni kama mnataka kuandika”.
Alipotafutwa jioni baada ya kuenea tetesi kwamba vikao vyote vitafanyika leo, hakupokea simu lakini alituma ujumbe mfupi wa maandishi ukisema: “Siwezi kuongea sasa… Samahani nipo kikaoni, tuma meseji”. Lakini hata alivyotumiwa ujumbe hakujibu.
Baadhi ya wajumbe wa Kamati Kuu walipoulizwa kikao chao kingefanyika lini, walisema hawakuwa na taarifa na kwamba na wao walikuwa wanasubiri kupewa taarifa.
Mmoja wa wajumbe wa NEC aliyekuwa akizunguka kwenye ofisi za makao makuu ya CCM, huku akionyesha amechoka, alisema: “Hapa nilipo hata sifahamu tutafanya lini kikao, nipo tu nazunguka hapa.”
Giza hilo ambalo limewakumba wagombea na wajumbe wa vikao, pia limesababisha kuenea kwa tetesi dhidi ya hatima za wagombea na kutoa fursa kwa wajumbe wenyewe kuzodoana.
“Mgombea wako keshamalizwa, kikao cha kamati ya maadili kimeshamkata,” ni miongoni mwa tetesi walizokuwa wakirushana roho wajumbe wa vikao vya CCM, ingawa taarifa za uhakika ni kuwa kikao hicho kilikuwa hakijafanyika.
Wengine waliokuwa na uelewa mpana walijibu kwamba vikao havijafanyika, hivyo kuhoji mgombea angekatwa na kikao gani.
Taarifa nyingine zilidai kuwa Kamati ya Usalama na Maadili ina dozi za baadhi ya wagombea maarufu na kwamba alama za ufaulu kwenye kamati hiyo zimewamaliza wengi.
Wagombea wanena
Pamoja na ratiba ya vikao hivyo kubadilikabadilika, makada waliojitokeza kuwania urais kwa tiketi ya CCM hawakuonekana kusumbuliwa na jambo hilo.
Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja alisema hana tatizo na kuchelewa kwa vikao hivyo kwa kuwa vina ratiba zake na maandalizi yapo ndani ya ratiba. Alisema viongozi wataendelea kutoa miongozo na anaamini msemaji wa chama ataendelea kuujulisha umma kinachoendelea.
Mgombea mwingine, Dk Hamis Kigwangalla alisema hakuwa na taarifa rasmi za kutofanyika kwa vikao kama vilivyopangwa, lakini akasema hilo halikuwa na madhara kwa wagombea na anaona sababu za kufanya hivyo ni kupunguza presha.
“Naamini vikao vyote vitakaa na chama chetu kuvisogeza mbele ni jambo la kawaida tumeshazoea. Nikiwa mmoja wa wagombea, sina shaka wala wasiwasi wowote, ratiba iliyopangwa ya vikao hivi imekutana na jambo kubwa.
Rais anatakiwa kuvunja Bunge na baadhi ya wajumbe watahudhuria shughuli hiyo, hivyo lazima visogezwe mbele,” alisema  mgombea mwingine January Makamba.
Mwalimu Banda Sonoko alisema kila kitu ni maandalizi hivyo anaamini kesho watakuwa wamepata mgombea, kwani vikao hivyo vimeingiliwa na mambo mengi, ndiyo maana vimesogezwa.
“Sina tatizo lolote, natambua mwenyekiti wangu pia ni Rais ana shughuli nyingi. Hili ni jambo zito, wahusika wanahitaji wasaa ili wasije kutupatia mgombea ambaye hafai, sidhuriki na hii chelewa chelewa, nitavumilia na kujigharimia kwa muda wote lakini tupate mgombea safi,” alisema Balozi Ali Karume.
Mjumbe wa kamati ya kampeni ya Lowassa, Hussein Bashe alisema hili siyo jambo la ajabu, bali ni kawaida kutokana na maelekezo ya chama vikao ni mpaka Julai 12.
“Kuahirisha vikao vya Kamati ya Maadili, Kamati Kuu na NEC siyo jambo la kutilia shaka,” alisema.
Msemaji wa Stephen Wasira, Masyaga Matinyi alisema anaamini kanuni, taratibu na katiba ya chama vitaheshimiwa hivyo mchakato utakuwa wa haki.
“(Wasira) Anaamini vikao vitafanyika kwa mujibu wa taratibu zilizopangwa, hivyo kuahirishwa huko hakuwezi kuvuruga mchakato,” alisema Matinyi.
Kada mwingine kwenye mbio hizo, Elidephonce Bilohe alisema anamwomba Mungu ili kuahirishwa kwa vikao hivyo kumpe neema kwa jina lake kupitishwa kuwa mgombea urais wa chama hicho.
“Jana (juzi) nilikwenda ofisi za CCM nikakutana na ofisa wa ngazi ya juu ya chama akaniambia kama tukihitajika na kikao chochote tutaitwa. Basi nikaondoka, nipo hapa nyumbani namwomba Mungu anisaidie niweze kuipata nafasi hii,” alisema Bihole.
Boniface Ndengo alisema kuahirishwa kwa vikao hivyo vya mchujo wa wagombea anaona hakuna tatizo.
“Nilishafanya sehemu yangu niliyotakiwa, sioni kama kuna usumbufu wowote,” alisema Ndengo.
Leonce Mulende alisema suala hilo halimpi matatizo ya kisaikolojia kwa sababu limewekewa programu za msingi, hivyo anafikiri watafikia hatima vizuri.
Balozi Patrick Chokala alisema: “Wenye shughuli zao ndiyo wanajua sababu za kuchelewa, wacha tusubiri watamaliza tu.”
Imeandikwa na Midraj Ibrahim, Noor Shija, Sharon Sauwa (Dodoma) na Suzan Mwillo (Dar).