TUTUMIE MAONI AU HABARI KUPITIA EMAIL: clickhabari@gmail.com AU SIMU: +255 7557 758 909, : CCM MBELE KWA MBELE 2015

NIA YA KUGOMBEA UBUNGE JIMBO LA ARUSHA MJINI MWAKA HUU 2015.

Ndugu Wana-Arusha na Watanzania kwa Ujumla,
Napenda kutumia fursa hii adhimu kuwatangazia kwa unyenyekevu mkubwa kwamba nitagombea Ubunge Jimbo la Arusha Mjini mwaka huu wa 2015. Kipekee nitumie fursa hii kumshukuru Mbunge anayemaliza muda wake (ndugu yangu, kamanda na mjomba wangu, Mhe. Godbless Lema) kwa kuwaongezea watu wa Arusha hali ya kuwa WAJASIRI; mimi nataka kuwapeleka mbele zaidi kwa kuwaonyesha na kuwafungulia milango ya fursa za kimaendeleo ili tusiishie kuwa wajasiri tu, bali sasa tuwe WAJASIRIAMALI na hivyo kujiletea maendeleo. Arusha ni jimbo lenye watu makini sana, wanachohitaji kwa sasa ni kiongozi mwenye maono, atakayewaonyesha njia sahihi ya kupita. Kiongozi huyo ni mimi.
Natambua kwamba jimbo lina watu wa matabaka tofauti na wenye itikadi tofauti na wakati mwingine zinazopingana sana, ila mimi nakuja kuwa Kiongozi wa watu wote bila kuangalia tofauti zetu. Nakuja kuwa baba, ambaye kwa kawaida, kama ana akili timamu na busara, huwalea watoto wake wote kwa upendo bila kuwabagua kwa vigezo vyovyote vile; na zaidi sana humkumbatia na kumbeba yule mtoto anayeonekana mnyonge, bila kukata tamaa, ili na yeye siku moja afanikiwe. Nakuja kuwa Mbunge na Baba wa Wana-CHADEMA na Wana-CCM (na vyama vingine vyote); Waislamu kwa Wakristo (na dini nyingine zote); wasomi kwa wasiosoma; maskini kwa matajiri; wanaosomesha watoto wao shule za kata (St. Kayumba) na wanaosomesha International Schools; wanaotibiwa ndani ya nchi kwa wanaotibiwa ughaibuni; wanaotembea kwenye barabara za lami na wanaotembea kwenye barabara za vumbi na tope; wanaoishi uzunguni kwa wanaoishi uswazi; wanaoishi kwenye nyumba za kupanga na waliokwisha kujenga nyumba zao; wanaofanya shughuli zao kwenye sekta rasmi na isiyo rasmi pia;

INAENDELEA.............

wakulima, wafugaji, waajiriwa, wafanyabiashara ndogondogo, za kati, kubwa, na zaidi sana wasio na ajira; wanaoendesha magari, bajaji, bodaboda, baiskeli, na wasiomiliki hata tairi la baiskeli; wanaojua shida ni nini na wale wanaosikia tu kwamba kuna msamiati unaitwa “shida”; wanaopata mlo mmoja kwa siku (na wakati mwingine hata kukosa kabisa) na wale wanaochafua meza; wanaowasha vibatari kwa wanaowasha umeme masaa 24; wanaoparangana kutafuta maji safi na salama na wale waliochimba visima majumbani kwao; wenye umri mkubwa, umri wa kati, umri mdogo na ambao wanategemewa kuzaliwa; wanaonikubali na wasionikubali; watakaonipa kura zao na ambao hawatanipa kura pia. Nakuja kuweka nguvu kubwa zaidi kwa watu wa hali ya chini ili nao wainuke na kuyafurahia matunda ya nchi yao hii nzuri, tajiri na iliyobarikiwa (Tanzania), kwani nao wana haki sawa na matajiri ndani ya nchi hii.
Natambua fika kwamba tuna changamoto nyingi na sio kazi rahisi sana kukabiliana nazo, ila nimejipanga kutumia uwezo na vipaji vyangu vyote alivyonipa Mungu kuhakikisha kwamba kwa pamoja tunazishinda. Nawaahidi kwamba nitasimama kwa ujasiri kukabiliana na kero zenu, na kamwe sitatetereka wala sitawaangusha. Niko tayari kushirikiana na madiwani wote ambao Mwenyezi Mungu atatupa bila kuangalia itikadi zao; na zaidi sana niko tayari kushirikiana kwa karibu sana na Rais yeyote ambaye Mungu atatupa katika uchaguzi mkuu ujao (sina kundi). Naamini ya kwamba mwaka huu Mungu atatupa viongozi wazuri sana na wenye majibu kwa matatizo ya Watanzania walio wengi.
INAWEZEKANA (IT IS POSSIBLE)…
Mungu ibariki Afrika, Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Arusha. Asanteni kwa kunisikiliza. Naomba kuwasilisha..
Ni Mimi Ndugu yenu,
Mosses Mwizarubi
23/05/2015.