Dodoma. “Anakatwa, hakatwi” ndilo swali lililokuwa linaulizwa
nchi nzima jana, lakini hatimaye Kamati Kuu ya CCM iliyokutana hadi
usiku wa manane iliibuka na jibu kwamba Edward Lowassa amekatwa, huku
kukiwa na wingu zito baada ya wajumbe watatu kupingana na uamuzi huo.
Muda mfupi baada ya kikao hicho, pamoja na kuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alikataa kutaja majina yaliyopitishwa, akaunti ya Twitter ya CCM, iliwataja waliopitishwa kuwa ni Bernard Membe, Dk John Magufuli, Dk Asha Rose Migiro, January Makamba na Amina Salum Ali na kuwatupa wengine 33 akiwamo Lowassa.
“Kikao cha Kamati Kuu kimeisha salama. Kesho (leo)
Halmashauri Kuu itakutana kuanzia saa 4:00 asubuhi,” alisema Nape baada
ya kikao hicho.
Alipotakiwa kutaja majina ya makada watano
waliopitishwa, Nape alisema: “Nimeambiwa mchakato bado unaendelea na
kesho (leo) Halmashauri Kuu itakutana kuendelea na kazi. Kwa hiyo
nawakaribisha kesho kuanzia saa 4:00 asubuhi mje mchukue picha, habari,
karibu sana.” Mkutano Mkuu utafanyika saa nane mchana leo.”
Dakika chache baada ya kikao hicho kumalizika,
wajumbe watatu wa Kamati Kuu, wakiongozwa na mbunge wa Songea Mjini, Dk
Emmanuel Nchimbi waliitisha mkutano na waandishi wa habari na kueleza
kuwa wanapinga uamuzi huo ambao hawakuutaja, wakidai kuwa si majina yote
yaliyowasilishwa mbele ya kamati hiyo.
Dk Nchimbi, akiongozana na mwenyekiti wa CCM wa
Mkoa wa Dodoma, Adam Kimbisa na mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania
(UWT), Sofia Simba waliwaeleza waandishi wa habari mara tu baada ya
mkutano wa Kamati Kuu kuwa kikao hicho hakikufuata kanuni kwa kuwa
majina machache yaliwasilishwa na hayakuhusisha mgombea anayekubalika.
Ingawa hawakumtaja mgombea huyo waliyesema anatajwa na wengi, wajumbe hao wanafahamika kuwa wanamuunga mkono Lowassa.
Baada ya kikao hicho taarifa za wagombea hao
zilisambaa kwa kasi katika mitandao ya kijamii na mijadala ya wazi
ilianza kuhusu uamuzi wa kumtosa Lowassa, ambaye alikuwa Waziri Mkuu wa
kwanza wa Serikali ya Awamu ya Nne.
Mmoja wa makada watano waliopitishwa kwenye mchujo
huo aliithibitishia Mwananchi kuwa jina lake limepita, lakini akasema
hataki akaririwe na badala yake akamshauri mwandishi aangalie akaunti ya
twitter ya CCM baada ya nusu saa.
Habari za jina la Lowassa kukatwa zilizagaa tangu
jana asubuhi, ilipoelezwa kuwa CCM ilifanya majadiliano na wadau
mbalimbali kuangalia jinsi ya kudhibiti watu wanaounga mkono baada ya
kupata taarifa kuwa ameenguliwa.
Lowassa azua mjadala
Awali wakati Kamati Kuu ya CCM ikikutana jana
usiku kupitisha majina ya makada watano walioomba kuwania urais, jina la
Edward Lowassa ndilo lililotawala mijadala mingi kwenye mitandao ya
kijamii, likiambatana na swali moja; amekatwa, hajakatwa?
Hali hiyo iliendelea zaidi jana usiku wakati CCM ilipotangaza
mabadiliko ya tatu ya ratiba za vikao vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu.
Watu wengi walikuwa wamefurika kwenye jengo la
makao makuu ya CCM mjini hapa, maarufu kama White House na walioruhusiwa
kuingia walikuwa waandishi wa habari na wajumbe wa Halmashauri Kuu na
Mkutano Mkuu, ambao walikuwa wakifuata makabrasha na vitambulisho.
Mapema jana, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM,
Nape Nnauye aliwaambia waandishi wa habari kuwa kikao cha Kamati ya
Maadili na Usalama ingekutana kuanzia saa 4:00 asubuhi na kufuatiwa na
Kamati Kuu saa 8:00 mchana, lakini baadaye akatangaza mabadiliko mengine
ambayo yalionyesha kuwa Kamati Kuu ingekutana kuanzia saa 10:00 jioni
na Halmashauri Kuu baada ya futari.
Majira ya saa 2:00 usiku, Nape alitangaza kuwa
kikao cha Kamati Kuu kingeanza muda huo na kwamba kingechukua muda mrefu
na hivyo Halmashauri Kuu itakutana leo kuanzia saa 4:00 asubuhi na
orodha ya makada watano waliopita kwenye mchujo itatangazwa muda huo.
Wakati Nape anawaambia waandishi wa habari jana
asubuhi kuhusu sababu za kuahirishwa kwa vikao, tayari kulikuwa na
habari kuwa Lowassa ameenguliwa baada ya vikao vya maridhiano kabla ya
vikao hivyo vya juu kuhusu namna ya kudhibiti wanachama wanaomuunga
mkono.
Habari hiyo ndiyo iliyokuwa mjadala mkubwa kwenye
mitandao ya kijamii. “Amekatwa au hajakatwa?” ndilo swali lililoulizwa
na wengi kwenye mitandao hiyo kutaka kujua kama kada huyo, aliyeonyesha
kuungwa mkono na wengi wakati wa kusaka wadhamini.
Akizungumza na waandishi jana asubuhi, Nape
alisema kuahirishwa kwa vikao hivyo muhimu kulitokana na mwenyekiti wa
CCM, Jakaya Kikwete kuwa na vikao na watu mbalimbali kupata ushauri
kuhusu namna ya kumaliza mchujo kwa usalama.
“Mwenyekiti alikuwa na vikao mbalimbali vya
consultation (mashauriano) na wadau ili kuhakikisha vikao vinakwenda
salama,” alisema Nape na kuongeza kuwa hiyo ndiyo ilisababisha ratiba ya
vikao kubadilishwa.
Hata hivyo, Nape hakuelezea vikao vya mashauriano kati ya Rais Kikwete na Serikali vilihusisha makundi gani.
Nape alisema mabadiliko hayo pia yalitokana na
shughuli za kiserikali na kichama ambazo Kikwete alikuwa nazo mjini
Dodoma, ambako Julai 9 mwenyekiti huyo wa CCM alifanya kazi mbili za
kuzindua jengo jipya la mikutano la chama hicho na baadaye kulihutubia
kwa mara ya mwisho Bunge la 10, siku ambayo alitakiwa kuongoza kikao cha
Kamati Kuu.
Awali Kamati ya Usalama na Maadili, ambayo
inachambua wagombea na kutoa mapendekezo ya kila mmoja, ilipangwa
kukutana Julai 8, na kufuatiwa na Kamati Kuu (Julai 9), Halmashauri Kuu
ya Taifa (Julai 10) na Mkutano Mkuu ambao ungefanyika Julai 11-12.
Lowassa ndiye anayeonekana kuwa kinara miongoni
mwa makada 38 walioomba kugombea urais kwa tiketi ya CCM, akionekana
kuwa na wafuasi wengi ndani na nje ya chama, hali ambayo aliionyesha
kwenye harakati za kutafuta wadhamini.
Mbunge huyo wa Monduli aliungwa mkono na takriban wenyeviti 15
wa mikoa, wabunge kadhaa waliojitokeza bayana kueleza misimamo yao kwake
na wajumbe kadhaa wa Halmashauri Kuu na Mkutano Mkuu.
Jana, baada ya kusogezwa mbele kwa kikao cha
Halmashauri Kuu, watu wengi waliondoka kwenye viwanja vya makao makuu ya
CCM, na hakukuwapo na makada wanaowania kugombea urais kwenye eneo hilo
ambako Kamati Kuu ilikuwa ikiendelea na kikao chake.
Kwa kawaida Kamati Kuu hupitisha majina matano kwa
makubaliano licha ya kwamba katiba ya CCM inaruhusu maamuzi kufikiwa
kwa kupiga kura.
“Mara nyingi hakuna upigaji kura kwenye vikao vya
Kamati Kuu,” alisema Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalum),
Profesa Mark Mwandosya alipoongea na Mwananchi nje ya jengo hilo jana
saa 2:40 usiku baada ya kuarifiwa kuwa kikao cha Halmashauri Kuu
kimeahirishwa hadi leo.
“Mara nyingi uamuzi huwa ni kwa maridhiano licha
ya Katiba kuruhusu upinzani kura pale mnaposhindwa kukubaliana,” alisema
Profesa Mwandosya ambaye alikuwa mjumbe wa Kamati Kuu.