Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete akiwa amewanyanyua mikono mgombea
urais kupitia chama hicho, Dk John Magufuli na mgombea mwenza wake,
Samia Suluhu Hassan mbele ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa chama hicho,
mjini Dodoma jana. Picha na Edwin Mjwahuzi
Dar/Dodoma. Mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk John Pombe Magufuli ameelezewa na watu mbalimbali kuwa ni mchapakazi, makini, asiyependa uvivu, lakini Rais Jakaya Kikwete amehitimisha yote kwa kumpachika jina la “tingatinga”.
Dar/Dodoma. Mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk John Pombe Magufuli ameelezewa na watu mbalimbali kuwa ni mchapakazi, makini, asiyependa uvivu, lakini Rais Jakaya Kikwete amehitimisha yote kwa kumpachika jina la “tingatinga”.
Rais Kikwete alisema hayo baada ya Magufuli
kutangazwa kuwashinda makada wengine wawili waliopigiwa kura na Mkutano
Mkuu wa CCM baada ya kuzoa kura 2,104, sawa na asilimia 87.08, ushindi
ambao alisema unaakisi kumalizika kwa makundi yaliyoibuka kwenye mbio za
kuwania kuteuliwa na CCM kugombea urais wa Serikali ya Awamu ya Tano.
Balozi Amina Salum Ali alishika nafasi ya pili kwa
kupata kura 253 (sawa na asilimia 10.4), wakati Dk Asha Rose Migiro
alikuwa wa mwisho kwa kupata kura 59 (asilimia 2.4). Jumla ya kura
zilizopigwa kwenye mkutano huo mkuu zilikuwa 2,422 na kura sita tu ndio
ziliharibika.
“Kila mtu anaitwa jembe,” alisema Rais Kikwete
alipokuwa akianza kutaja sifa za Magufuli ambaye amewahi kuwa Naibu
Waziri wa Ujenzi na pia Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi.
“Lakini huyu ni zaidi ya jembe. Ni tingatinga…
Magufuli ni bulldozer. Magufuli havumili ujinga, ni mtu ambaye anataka
kuona kazi zake zinafanyika kama alivyoagiza.”
Kikwete aliendelea kummwagia sifa Dk Magufuli
kuhusu utendaji wake akisema kuwa alipokuwa akifuatilia wakandarasi
kwenye miradi ya ujenzi, alidiriki kuwatimua pale alipobaini walikuwa
wakifanya kazi kinyume na makubaliano.
“Tunaamini kuwa utawaongoza Watanzania vizuri,” alisema Kikwete akimgeukia mbunge huyo wa Chato.
“Tulikuwa na wagombea 338 lakini sasa tunaye mmoja
na tuna kundi moja tu la CCM. Timu Magufuli imeshaondoka. Wengi
walidhani CCM itafia hapa, lakini ushindi huu ni ishara kuwa CCM ni
moja.
“Tunatakiwa kuacha kuteuwa watu kwa urafiki na
kujuana ili tushinde kwa sababu imani huzaa imani. Sina shaka kuwa
tutashinda lakini ushindi hauji hivi hivi lazima tuwe na mikakati
mizuri, mipango thabiti na utekelezaji makini,” alisema.
Rais Kikwete ni mmoja kati ya watu wengi
waliohojiwa na Mwananchi kuhusu mteule huyo wa CCM, ambaye hakuwa
akitajwa kama kinara kwenye mbio za urais kabla ya kufikia hatua hiyo ya
kujadiliwa na vikao vya juu.
Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Mhandisi Mussa
Iyombe, aliyefanya kazi na Dk Magufuli kwa zaidi ya miaka 10, alisema
iwapo atachaguliwa kuwa rais basi wavivu wajitayarishe kukimbia kwani
Waziri huyo ni mchapa kazi wa hali ya juu.
Iyombe alisema kwa kipindi alichofanya kazi na
Magufuli ameshuhudia kuwa hataki mchezo katika kazi, hana mzaha na
mwenye umakini mkubwa kwa kila anachofanya.
“Ninachoweza kusema ni kuwa huyu hataki mchezo, kwa hiyo wale
wavivu wavivu najua watashindwa kuendana na kasi yake ya utendaji kazi,”
alisema.
Iyombe alimmwagia sifa Magufuli kuwa hapatani na
wazembe na wavivu, jambo ambalo alisema liliwahi kuwakimbiza baadhi ya
wahandisi walioajiriwa wizarani hapo.
“Tangu alipoingia wizarani 2005, kama naibu waziri
alianza kufanya kazi vizuri, sina sifa zaidi kuwa ni mchapa kazi,
hawezi kuwa na upendeleo kulingana kabila, wala undugu. Hajali kitu,
ukiharibu kazi atakuponda tu,” alisema.
Msemaji wa Wizara ya Ujenzi, Segolena Francis
alimsifu Magufuli kuwa ni mtu anayejali muda, anayependa kazi yake na
asiyetaka mtu legelege.
“Nimejifunza mambo mengi kwake na ninatumaini kuwa
kama atakuwa Rais, basi Taifa litakuwa limepata mchapakazi. Anafuatilia
kila kitu yeye mwenyewe, hana makundi, hana ukabila wala udini,”
alisema.
Segolena alisema Magufuli ni miongoni mwa viongozi
ambao hawapendi kupindisha mambo na wanataka kila kitu kiende kama
kilivyopangwa.
Aliyesoma naye alonga
Sifa kwa Dk Magufuli pia zilitolewa na
Ndyesumbilai Florian, mmoja wa watu waliosoma naye Shule ya Sekondari ya
Katoke Biharamulo na ambaye sasa ni mhariri msanifu wa gazeti la
Mwananchi.
“Magufuli aliwahi kusema kuwa siku moja atakuwa
kiongozi mkubwa na hivyo ndoto hizo zinaweza kutimia baada ya kuteuliwa
kuwania urais kupitia CCM,” alisema Ndyesumbilai.
Ndyesumbilai alisema hata walipokuwa kidato cha
tatu, Magufuli alizungumzia nia ya kugombea Jimbo la Biharamulo wakati
huo likishikiliwa na Chief Kasusula.
“Nafikiri aliwahi kugombea lakini hakufanikiwa,
lakini mara kadhaa alikuwa akisema kuwa anatamani majimbo ya ubunge
yashikiliwe na vijana,” alisema.
Ndyesumbilai alieleza zaidi kuwa hata baada ya
kufanikiwa kuwa mbunge wa Chato, bado Magufuli aliendelea kusema kuwa
safari ya uongozi bado ni ndefu kwake.